Monday, February 5, 2018

SIMULIZI; TUSISAHAU TULIPOTOKA

*** Kisa hiki kimenigusa sana  na nampenda sana Mama yangu hata kama ameshatangulia mbele za Mungu, hakuna kama mama.....haya ndugu yangu hebu twende sambamba nami**** KARIBU

Binti mmoja ambaye alitokea katika familia masikini alifanikiwa kusoma kwa shida mpaka kufanikiwa kuwa mwanasheria. Alipata kazi nzuri, akiishi katika nyumba nzuri ya kifahari.

Pamoja na maisha mazuri lakini binti aliwasahau kijijini kwao, alikua akituma pesa kidogo lakini hakutaka kwenda. Alitaka kuyasahau maisha yake yote ya mateso ya kijijini.

Hata kwa marafiki zake alijitambulisha kama kazaliwa Dar huku akidanganya kuwa wazazi wake wamefariki na yeye alikua ndiyo mtoto pekee, hii ni kwasababu marafiki zake wote walikua wakitoka katika familia za kitajiri.

Baada ya kukaa muda mrefu bila kufika kijijini kwao wazazi wake walipata wasiwasi, huku wakiwa na wasiwasi kuwa kuna kitu kimempata, walichangisha nauli na Mama yake ambaye alikua mzee sana alipanda gari na kwenda kumuona mjini.

Alipelekwa na jirani yao mmoja ambaye alikua akifahamu alipokua akiishi yule binti. Mama alifika na kukuta binti akiwa na afya nzuri, hana tatizo lolote. Binti alikasirika sana kumuona mama yake kwani alikuja bila taarifa.

Hakumsalimia vizuri na kila saa alikua akimlaumu kwanini hakupiga simu kwanza na kama ni hela si angesema amtumie. Mama huku akitokwa na machozi ya furaha alisema shida yake haikuwa hela bali kumuona mtoto wake baada ya muda mrefu.

Binti alimdanganya mama yake kua ile nyumba ni nyumba ya kampuni hivyo haruhusiwi kuishi na mtu yoyote kutokana na kazi aliokuwa anaifanya hivyo yeye asingeweza kuishi pale.

Mama hakuwa na maneno, alimuambia hamna shida yeye kwa kuwa alikwisha muona mwanae roho yake imetulia kwani hakwenda kukaa pale alikwenda tu kumuona.

Binti alimuacha mama yake apumzike siku ile na kesho yake ili siku inayofuata apande gari kurudi kijijini. Siku iliyofuata baada ya kutoka kazini rafiki zake walikuja, kulikua na sehemu ambayo walishapanga kwenda.

Walimkuta mama yake akiwa nje akipunga upepo. Walimsalimia vizuri na binti alipowaona aliwakimbilia kuwawahi ili Mama asijitambulishe, alifika na kuwaharakisha rafiki zake ili waondoke.

Walipotaka kujua ni nani, alijikuta anadanganya “ Huyo mama amepotea njia, alipita hapa alikua anamtafuta mtoto wake akakosea nyumba, sasa ndiyo namsaidia, aligonga kwangu kuomba simu, kwani alikua na namba ya mwanae kwenye kikaratasi.

Nimeshampigia mwane atakuja kumchukua. Binti alionge akiamini kuwa kesho yake anamuondoa mama yake mule ndani hivyo rafiki zake hawatamuona tena.

Wakati akiongea yale maneno hakujua kuwa mama yake anasikiliza, alistuka baadaye alipogeuka wakati anafungua mlango wa gari ili aingie. Mama yake alikua anatokwa na machozi, binti alijikaza kama vile hakumona akaingia kwenye gari na kuondoka.

*****
Baada ya mizinguko yake binti alirudi nyumbani, hakumkuta mama yake, alimuuliza mfanyakazi wa ndani akasema hajui, alijua wameondoka wote kwani alimuacha nje wakati yeye anatoka na gari.

Binti alianza kupaniki, alisubiria mpaka usiku wa manane lakini mama yake hakurejea. Hapo alianza kuchanganyikiwa, kichwa kikikumbuka maisha ya shida waliyopitia, namna ambavyo Mama yake alivyoteseka kwaajili yake.

Machozi yalinza kumtoka akijutia mambo aliyomfanyia mama yake. Alimtafuta yule kaka ambaye alimleta mama yake pale lakini hakuwa akijua chochote. Usiku ulipita akiwa macho, asubuhi alilazimika kwenda kazini kwani alikua na kikao.

Lakini mchana alishindwa kuvumilia, ilibidi kwenda polisi na kuanza kumtafuta mama yake lakini hakupatikana. Siku moja ilipita na hatimaye ya pili ilipita bila kumuona mama yake, alianza kuwa na wasiwasi.

Akiwa ofisini hajui hili wala lile rafiki yake mmoja alikuja, walianza kuongea akiwa hana raha kabisa. Rafiki yake alimuuliza tatizo lilikua nini akaamua kumuambia, lakini kabla hajaanza kuonge rafiki yake alisema.

“Halafu shogaa nilitaka kusahau, unamkumbuka yule bibi ambaye tulimkuta kwao jana?”
“Ndiyo namkumbuka! Amefanya nini? Umemuona wapi?” Alijikuta anadakia kwa haraka kutaka kujua.
“Basi jana wakati natoka kazini nikapita sehemu, nimekuta watu wamezunguka, kumbe kagongwa na bondaboda kaumia kichwani, watu wakawa wanakimbia kukwepa ushahidi.

Na mimi nikapita, sasa baadaye narudi kumbe watu walimuacha pale bibi wa watu mpaka polisi wanakuja lisaa lizima baadaye basi bibi wa watu amesha fariki. Kusema kweli roho iliniuma sana kwa kumpita bila kumsaidia…”

Rafiki yake aliongea kwa masikitiko, lakini kabla hajamalizia yule binti alidondoka na kupoteza fahamu. Alizinduka yuko hospitali kazungukwa na marafiki zake na mchumba wake.

Walimuuliza sababu ndipo alipoamua kuwaelezea, kila mtu alimshangaa kwa kumficha mama yake, walihangaika kumtafuta wakakuta maiti yake, wakamsaidia kusafirisha maiti mpaka Kijijini. 

Walizika salama lakini baada ya kurudi mchumba wake alimuacha, marafiki zake wote aliokuwa akiwaona wa maana walimtenga kutokana na tabia zake. Binti alishikwa na msongo wa mawazo.

Kila siku ilikua akilia tu, alishindwa kufanya kazi vizuri, sasa hivi amefukuzwa kazi. Kahama nyumba ya kifahari aliyokua akiishi na sasa yuko mtaani akitafuta ajira huku akiona hata aibu kurudi nyumbani kuwaona ndugu zake.

No comments: