Wednesday, February 3, 2010

Mapotopoto: Matunda pori yenye sifa tatu

mti wa masuku/mapotopoto
matunda kwenye mti (masuku) mapotopoto


Habari hii imenikumbusha nilipokuwa mtoto magauni yalikuwa yanachanika mpaka mama alikuwa anachukia kweli. Maana ukienda porini ukirudi mapotopoto kibao kwenye gauni. Sielewi kwa nini nilikuwa sichukui kapu. Haya ungana nami tusome:-)

*Utamu wake wamithilishwa na asali
*Miti yake yadaiwa kutibu malaria
*Magamba yake ni mbolea maridhawa

RUVUMA ni mkoa uliojaliwa neema nyingi. Una aina mbalimbali za madini na inaelezwa kwamba utafiti wa kina ukifanyika unaweza kuwa na migodi mikubwa hivyo kuinua uchumi na ajira.
Katika sekta nyingine, Ruvuma ina misitu mikubwa iliyosheheni miti ya aina mbalimbali. Pia una Ziwa Nyasa lenye samaki watamu na dagaa wazuri kuliko dagaa wowote nchini.
Vile vile Mkoa wa Ruvuma una mito mingi, Mngaka, Ruhuhu na Ruvuma, kutaja michache, inavutia na inatoa samaki watamu kama mbasa, mbufu, mbelele na wengineo. Ruvuma ni moja ya mito mikubwa nchini na ambao unatenganisha Tanzania na Msumbiji.
Mkoa huo una milima ya kuvutia ambayo kama ikifanyiwa kazi inaweza kuwa moja ya vivutio vya kitalii na kuliingizia taifa na vijiji vinavyoizunguka kipato.
Milima Mara kwa mfano, uliopo Kata ya Magagura, unaweza kuwa kivutio kutokana na urefu na mandhari yake. Pia ipo Milima ya Litenga iliyotegwa na maji ambayo inalisha vijiji zaidi ya saba kwa miaka zaidi ya 30 sasa. Kuna safu ya Milima ya Livingstone, kuna Jiwe la Mungu huko Mbinga.
Pamoja na sifa hizo nilizotangulia kuzitaja, Mkoa wa Ruvuma una sifa nyingine kubwa inayotambulika zaidi hata kwa wanafunzi wa shule ya msingi, kilimo.
Mkoa huu ni moja ya mikoa minne 'the Big four' inayolisha chakula Tanzania na nchi za jirani. Pamoja na kuwa kilimo cha mahindi kinacholimwa zaidi Wilaya ya Songea, Ruvuma inazalisha kwa wingi mpunga, ulezi, ufuta, mtama, mihogo na soya.
Mbali ya mazao hayo ya chakula, kuna mazao ya biashara kama vile kahawa inayolimwa na kustawi zaidi wilayani Mbinga, na korosho inayolimwa zaidi Tunduru.
Sambamba na mazao ya chakula na biashara Ruvuma pia ina aina mbalimbali za matunda, ya kupandwa na yapo pia ya asili yanayopatikana kwa wingi misituni. Matunda pori haya yanajulikana kama mapotopoto, pia huitwa masuku.
Matunda mengine yanayostawi kwa wingi katika hasa katika Wilaya za Songea na Mbinga ni yake yanayojulikana kama Matunda Mungu.
Katika matunda yote hayo, mapotopoto yanaongoza kwa sifa. Wenyewe wanayafananisha na asali kwa utamu. Tunda lake lina mbegu nne ndani yake zinazozungukwa na utando wenye rojorojo ambao ndio hasa unaonywewa. Msimu wake wa mavuno ni kila robo ya mwisho wa mwaka.
Matunda haya yamekuwa chanzo kizuri cha ajira kwa akina mama wengi kwani wakati wa msimu, huenda porini na kwenda kuyauza katika maeneo mbalimbali kama vile kwenye vituo vya mabasi, sokoni, na wengine wakitembeza mitaani.
MMoja wa wachuuzi wa matunda hayo, Flora Mhagama anasema wakati mwingine huuza ndoo nzima kwa siku lakini kutokana na wingi wake porini, watu wengi huyafuata hivyo kufanya bei yake kuwa ndogo.

Anasema kwa ndoo hiyo moja anaweza kuingiza kati ya Sh1,000 na 1,500. Anauza kwa kupanga mafungu na kila fungu huuza kwa Sh50... “Yanatusaidia kupata fedha ya chumvi na sabuni.”
Wenyeji pia wanaamini kwamba miti inayotoa matunda hayo huweza kutoa dawa ya kutibu malaria inapokuwa michanga. Hii ni changamoto kwa watafiti wa dawa za tiba kubainisha ukweli huo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Wilaya ya Songea Vijijini Rogatus Haule anasema amewahi kusikia fununu hizo.
“Nimewahi kusikia kuwa miti michanga huweza kuwa dawa ya malaria ila siwezi kuthibitisha kama ni kweli au la. Ni ni wakati muafaka kwa taasisi za serikali na binafsi zinazojihusisha na utafiti wa dawa kutopuuzia fununu hizi na kuifanyia utafiti mimea hiyo,” anasema.
Inaelezwa pia kwamba masalia ya maganda ya matunda hayo ni rutuba nzuri kwa zao la uyoga. Hiyo inathibitishwa na ukweli kwamba katika misitu ambayo mapotopoto huzaliana kwa wingi, uyoga pia huota na kustawi.
Tatizo lililopo katika biashara ya matunda hayo kama ilivyo kwa mazao mengi mengine ni soko. Kwa mfano, Mkoa wa Dar es Salaam ambao hauna msimu wa matunda haujawahi kupelekewa mapotopoto.

Tatizo la kutopanua soko na kuangalia uwezakano wa kuyasindika matunda hayo ni moja ya changamoto ambazo zinawakabiliwa wadau wa kilimo wa Mkoa wa Ruvuma.

Na Jacob Malihoja kutoka gazeti la mwananchi

11 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Ngoja nifunge mjadala, mwenga wangoni vayangu muvi kwoki mkosiwi mapotopoto cha kuniga. Ok ngoja nandika kwa lugha ambayo wote tutaelewa, mwenzenu haya mapotopota ninayapenda mno mwaka jana nilipokuwa nyumbani ulikuwa ndio msimu wake wacha niyale...raha kweli nasikitika sikuweza kula (madonga) ni matunda pori pia haya ni ya mviringo ukubwa kama embe dodo ila mviringo kwanza yanakuwa kijani na yakiiva yanakuwa njano unamungúnya mbegu zake kama pipi vile. Naweza kusema ni pipi za kienyeji. Nayapenda sana maisha ya vijijini.

Lulu said...

Yasinta ungemuomba mtu aliyeko Songea akutumie picha utuwekee maana inawezekana hata vijijini kwetu yapo isipokuwa yana majina tofauti.

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

@Lulu: hapo uminena kwani pamoja na jina hilo nadhani nayajua haya matunda.

Yasinta: yakiiva yana rangi gani na yakiwa machanga yanakuwaje? yana utomvu?

Kwa kweli miye napenda sana kula matunda pori kuliko haya ambayo yamebadilishwa vinasaba (genetically modified) tunayonunua kwenye masupamaketi.

Koero Mkundi said...

Siju ndio yale tunayoyaita matopetope kule upareni?

Labda kama utatuwekea picha, maana nahisi kama nimeshayala hayo matunda,

We chacha Musoma kuna matunda au Kilimo cha Bangi!!!??LOL

Koero Mkundi said...

Siju ndio yale tunayoyaita matopetope kule upareni?

Labda kama utatuwekea picha, maana nahisi kama nimeshayala hayo matunda,

We chacha Musoma kuna matunda au Kilimo cha Bangi!!!??LOL

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

@Koero: bangi sunna shosti :-)

kwa taarifa yako Iringa wanailamba kama hawana akili nzuri in the name of mboga na kwa Musoma ni zao zuri la biashara.

Imagine ekari moja unapewa 1,000,000 cash kabla hata hujaanza kulima.

je wajua kuwa 'viongozi' wetu pia wanashiriki kulima? :-(

hata huko upareni mnalima sivo? :-(

Simon Kitururu said...

Hapa picha ingekuwa Msaada sana. Ingawa nimewahi kuishi Ruvuma, [Songea nilikosomea shule ya vidudu na kuanza shule ya Msingi Mfaranyaki] Sina kumbukumbu Mapotopoto ndio nini.:-(

Ila kwa bahati mbaya sipendi asali labda ndio sababu siyajui!:-(

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

eeh! huo naujua. ntaulizia kwa kikonongo unaitwaje kisha ntarejea kuonana nanyi

Yasinta Ngonyani said...

Ok ndugu zangu sasa nimeipata picha nimeagiza kutoka songea na kwa haraka kabisa tayari nimeipata nadhani sasa wote mtaweza kujua ni matundu gani gani haya MAPOTOPOTO/MASUKU. KILA LA HERI , UPENDO DAIMA!!

Upepo Mwanana said...

Tembelea blogu ujifunze mengi. Hayo matunda sijawahi kuyasikia!!

Jacob Malihoja said...

Dada Yasinta,

Nimefurahishwa sana na kitendo chako cha kuweka makala yangu ya Matunda ya mapotopoto kwenye Blog Yako. Kwa niaba yangu binafsi, kwa niaba ya watu wa mkoa wa ruvuma na kwa niaba ya taifa kwa ujumla ninakushukuru kwa kitendo hicho.

Lengo la kuandika makala ile ni kiubua uwezekano wa matunda hayo kupata soko jijini Dar na katika miji mingine mikubwa pamoja na nje ya Tanzania ili kuwaongezea uchunmi wananchi wa mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla. Nakushukuru kwakuwa kitendo chako ni kuunga mkono mtazamo wangu na ikiwa kutakuwa na mafanikio siku moja utakuwa na kila sababu na wewe kujisikia kuwa umehangia mafanikio hayo.

Aidha natumia fursahi hii kukusishi wewe na mabloger wote wa kitanzania kuibua vitu ambavyo sio tu vitakuwavinachangamshi, kuelimisha lakini pia vitu ambavyo vinaweza kuchangia maendeleo ya taifa letu masikini.

Aidha nakupongeza kwa kazi zako nyingi, ingawa sijapata muda wa kutosha lakini chache nilizopitia nimependezwa. Nawapongeza pia wasomaji wako na wana blog wenzako.