Tuesday, February 21, 2017

UJUMBE KUTOKA KWANGU KUJA KWENU

Kabla hujadhani, jifunze ukweli kwanza. 
Kabla hujahukumu , elewa kwanza ni kwanini.
Kabla hujamuumiza mtu, hisi kwanza. Na 
Kabla hujazungumza/sema, fikiri kwanza
NAWATAKIENI WOTE SIKU NJEMA NA KILA MUFANYALO LIWE JEMA!

Friday, February 17, 2017

TUMALIZE WIKI HII KWA HII:- ENZI HIZOOO

AU TU TUMSIKILIZE NA PWANGUZI NA PWANGUZI Nakumbuka hiki kipindi kilikuwa hakinipiti kabisa...Je? ww wenzangu unakumbuka? TUSISAHAU KUWASIMULIA VIZAZI VYETU AU TU KUSIKILIZA PAMOJA:-) IJUMAA NJEMA!

Thursday, February 16, 2017

WAMETOKA SASA HIVI ZIWANI. ...

Nimekumbuka kwetu Nyasa samaki kila siku....

Monday, February 13, 2017

JUMATATU HII IANZE HIVI:- JIKONI LEO UGALI

 Ugali, mchanganyiko wa maharege na viazi  pia matembele
...na hapa ni ugali na mboga iliyoungwa karanga...
Binafsi nachagua ule mlo wa kwanza maharage na matembele kwa vile SIPENDI KABISA MBOGA au CHAKULA CHOCHOTE KILICHOWEKWA KARANGA....Ndiyo maana nimeandaa aina mbili isije nikashinda njaa:-)

Sunday, February 12, 2017

UNGEKUWA WEWE UNGEFANYA NINI....JUMAPILI NJEMA!

Kweli hapa kuna haja ya kuwita baba  maana hakuna jinsi. NAWATAKIENI WOTE MTAKAOPITA HAPA JUMAPILI YENYE AMANI NA FURAHA.

Saturday, February 11, 2017

SIKU MBAYA (Jifunze kupitia simulizi hii)

Nimeamka asubuhi hii na kukutana na simulizi hii katika barua pepe yangu. Baada ya kusoma nikaona ni simulinzi nzuri na ya kufundisha  katika maisha ya kila mwanajamii. Kwa hiyo nikaona niiweke hapa kibarazani kwetu ili  kwani elimu hawanyimani...karibuni 
Kijana akiwa katika maombi
Ilikuwa ni saa moja na nusu saa za asubuhi ambapo kijana aitwae John alikuwa ndo anaamka.
Mara baada ya kuamka na kukamilisha ratiba yake ya asubuhi ikiwemo kuoga, kupiga mswaki na kupata kifungua kinywa kijana alienda alipopaki gari yake tayali kwaajili ya kuelekea ofisini. Ile anataka kuwasha gari yake ghafla engine ikagoma kuwaka. Akashuka kwenye gari yake na kuamua ketembea kwa miguu mpaka kituo cha mabasi. Hata hivyo baada ya kufika kituo cha mabasi hakufanikiwa kupanda basi kwa kuwa mabasi yote yalikuwa yamejaa.

Ili asichelewe kazini kijana akaamua kukodi tax. Akiwa ndani ya tax alipigiwa simu na mmoja kati ya washirika wake kibiashara lakini kabla hajapokea simu ikazimika na hata alipojaribu kuiwasha akagundua betri ilikuwa imekufa. Akiwa bado yupo ndani ya tax mwendo kidogo baadae tax nayo ikazimika ghafla na haikuweza kuendelea na safari. Akamlipa dereva tax pesa yake na kuamua kukodi tena pikipiki (bodaboda) ambayo ilimfikisha mpaka kazini kwake. 

Kabla hajaingia ofisini kwake mtu mmoja akataka kumshika mkono na kumpongeza kwa promotion ambayo ilitakiwa kufanyika siku hiyo.
Lakn kabla hajafanya hivyo akaitwa na mtu kwa nyuma ambaye baadae akamwambia kwamba promotion ilikuwa imeahilishwa.

Jioni baada ya kufika nyumbani kijana akaanza kunung'unika huku akisema:
"mambo gani haya!!!"
"kwanini leo imekuwa SIKU MBAYA kwangu kiasi hiki!!"
"Ee Mngu nimekukosea nini mimi mpaka siku yangu iwe mbaya kiasi hiki!!" 
Mara ghafla akasikia sauti ya Mumgu ikisema:
"Asubuhi ulipowasha gari yako ikagoma kuwaka mm nilihusika kwa sababu ungepata ajali mbaya sana kama ungetoka na gari yako leo"
Ulipotaka kupokea simu betri ikafa mm nilihusika kwa sababu aliyekupigia simu alitaka kukupatia taarifa za uongo ambazo zingepelekea kuharibu uhusiano kati yako na wafanyabiashara wengine.

Hatua chache baadae tax ilishindwa kuendelea na safari kwa sababu yule dereva tax ni agent wa kikundi cha wateka nyara hivyo kama mngeenda mbele zaid huko angebadili mwelekeo na kukupeleka chini ya jengo moja kubwa ambalo limekuwa likitumika kwa shughuli zao za uharifu na hatimae wangekuteka.

Ulipofika ofisini nilizuia mtu mmoja asikushike mkono kwa sababu nilikuwa nakuepusha na maambukizi ya ebora kwani yule mtu amesha ambukizwa vurusi vya ugonjwa huo

Baadae kidogo ile promotion ambayo ulitegemea ikuingizie pesa nyingi sana ukaambiwa imeahilishwa hapo napo mimi nilihusika kwa sababu kuna mtu hakufurahia ww kupata nafasi ile hivyo akaamua kupandikiza mapepo kwenye kiti ulichotakiwa kukalia ndani ya ukumbi ambapo mapepo hayo yangepelekea kifo chako.

Sasa hebu niambie 
-Siku ya leo ilikuwa mbaya kwako
-Na je yote niliyokutendea yalikuwa mabaya?Kijana kusikia hivyo alilia sana,akajilaumu kwa jinsi alivyo mnung'unikia Mungu. Akapiga magoti akatubu,  hukuakimshukuru Mungu.
-------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
Ninachotaka hapa uelewe ni kwamba upo hai leo ni kwa sababu Mungu amependa uwe hai na ana makusudi na maisha yako.

Wakati mwingine kuna mambo mabaya huwa yanatokea katika maisha yetu yanayotufanya tuone kama Mungu ametusahau.
Tunamnung'unikia na kumlaumu Mungu bila kujua kuwa Mungu ana njia nyingi sana za kutuepusha na mabaya.
Wakat mwingine tunasahau kuwa mabaya tunayokutana nayo yanafanya kazi kwa Manufaa ya hatma zetu.

Unaweza fukuzwa kazi usijue kumbe ndio unaelekea katika kazi bora zaidi,
Unaweza kuachwa na mtu uliyempenda sana ukadhani ndiyo mwisho wa maisha kumbe Mungu amekuandalia mtu mwingine mwenye mapenzi ya dhati mtakayefikia malengo ya kujenga familia,
Unaweza kukataliwa na kutengwa na ndugu kumbe Mungu amekuandalia watu-baki watakaofanikisha ufikie malengo yako pasipo masimango ya ndugu,
Unaweza kuona marafiki wanakusariti kumbe Mungu anawaondoa makusudi ili kukuepusha na mabaya waliyoyapanga juu yako.  

MWISHO naomba nikuhakikishie kwamba Mungu anayaona matatizo yako na kwa hakika hatoacha yakuangamize bali atakwenda kufanya njia ya kutokea ktk magumu yote unayopitia.
Kama unaamini kwanini usiseme AMEN.

Thursday, February 9, 2017

BLOGG YA MAISHA NA MAFANIKIO IMECHAGUA HII PICHA KUWA PICHA YA WIKI....

Hakuna kupoteza muda hapa...nimeipenda hii safi sana UMOJA NI NGUVU UTENGANO NI UDHAIFU....AU MNABISHA?

Tuesday, February 7, 2017

SEHEMU FULANI TANZANIA

Je? unajua hapa ni wapi katika nchi yetu ya Tanzania?....zawadi nono imeandaliwa:-)

Monday, February 6, 2017

LEO NIMEYAKUMBUKA MATUNDA HAYA ADIMU MATUNDA DAMU/TAMARILLO

Mti wa matunda damu/tamarillo ukichanua
 Hapa tayari yameiva
Mavuno tayari. 
Kama nilivyosema kwenye kichwa cha hapo juu haya matunda ni adimu na pia ukiyapata ni ghali sana..Inabidi nianze kulima .... JUMATATU/MWANZO MWEMA WA WIKI !!

Sunday, February 5, 2017

VAZI LA JUMAPILI YA LEO KITENGE CHENYE ASILI YA TANZANIA....JUMAPILI NJEMA


MDADA LEO KATOKA KITANZANIA HASWA...ANGALIA KITENGE
Kwa mbali anaonekana kuchoka choka lakini ...ni vazi la jumapili ya leo kitenge chenye maandishi ka nitokako TANZANIA.
JUMAPILI NJEMA KWA WOTE WATAKAOPITA HAPA NA PIA JIONI/MCHANA NA USIKU MWEMA KWA WOTE.

Monday, January 30, 2017

JIKONI LEO...KUOKA MIKATE

 Hii ni kazi ya mikono yangu...huwa napenda kuoka mikate mwenyewe kwa hiyo leo nimeoka ...hapa imekwisha umuka....
.....baada ya dakika 12 kwenye oveni tayari ....karibu  wale wapenzi wa mikate mimi napendaga magimbi bwana:-)

Friday, January 27, 2017

KUMBUKUMBU...JINSI YA KUPATA POMBE YA ULANZI

Kuhusi Ulanzi:- Kwanza nakumbuka nilipokuwa msichana mdogo bibi na babu yangu walikuwa na "vitindi" miti ya ulanzi mingi sana na walikuwa wakiuza sana ulazi ...na baada ya miaka nikawa naishi Madaba-Matetereka kule nako kulikuwa na ulazi mwingi sana ...ila bahati mbaya au nzuri sijui utamu wa ulanzi...sijawahi kuonja:-)...NAWAPENDA WAOTE NA NAWATAKIENI MWISHO MWEMA WA JUMA HILI...USIBUGUE SANA ULAZNI:-).....KAPULYA

Thursday, January 26, 2017

MBUZI WA AJABU MPAKA JUU YA MTI...

Binafsi sijawahi kuona  mbuzi wakipanda juu ya mti...yaani wamenipita hadi mie:-) kaaaazi kwelikweli

Tuesday, January 24, 2017

KATUNIYETU YA LEO... MANENO YA WATOTO!....

 ...NAWATAKIENI WOTE SIKU NJEMA !PANAPO MAJALIWA

Monday, January 23, 2017

ZILIPENDWA..UNAKUMBUKA HIVI?

FANTA SIO FANTA TU  BALI HAZIKUWA ZIKICHAKACHULIWA
Nakumbuka sana haya makopo vilikuwa na ubora sana hivi vitu, siku hizi duh! kaaazi kwelikweli...sijui  wenzangu mnasemaje?

Thursday, January 19, 2017

SWALI LA LEO: SISI BINADAMU NI KITU GANI HASA?

Tunajitahidi sana katika kuvaa vizuri, kula vizuri, kujenga nyumba bora, kendesha magari makubwa na kufanya mengine ambayo yanaweza kuipa raha miili yetu na kutupatia  umaarufu ikibidi. Moja ya sababu za kufanya kwetu hivyo, ni ile imani yetu kwamba sisi ni miili yetu. Lakini ajabu ni kwamba, pamoja na kufanya hivyo, bado tunajikuta haturidhiki. Wengi hatujui kwamba, kutoridhika kwetu huko ni taarifa kwamba sisi ni kitu kingine, siyo miili hii tuliyonayo. Je, tumeshawahi kujiuliza sisi ni akina nani hasa? Kama bado, tumepata nafasi ya kujiuliza sasa na bila shaka tutapata jibu litakaloturidhisha.
Chanzo:- kitabu cha MAISHA NA MAFANIKIO

Wednesday, January 18, 2017

PALE NDUGUZO NA MARAFIKI WANAPOKUTAMANISHA CHAKULA /VYAKULA UVIPENDAVYO:-)

Ugali wa ulezi  kwa kuku(mawondo ni kingoni) paja na mchuzi. utadhani mlima Kilimanjaro ukiisha huo itabidi kupumzika haswaaa
 Kuna mdogo wangu anajua sana mimi ni mpenzi sana wa ugali  kanitumia hii ili nitamani na kweli nimetamana...ugali na dagaa ...
....na mwingine kunitamanisha hiii wali, kuku na mboga mboga ...:-) watu wachokozi sana kwa kweli

Tuesday, January 17, 2017

USIHANGAIKE, FANYA MAMBO YAKO KWA UBORA NA USHUKURU KWA KILA HATUA KISHA SAHAU MENGINEYO

Tupo wengi sana tunaofikiri hivi:-Ya kwamba kuna mambo mengi sana tunapitia katika maisha yetu ya kila siku mengine mazuri, na mengine mabaya na wakati mwingine tunakutana na watu wazuri ambao wana tufurahisha lakini wakati huohuo yawezekana ukakutana na mtu ambaye akakuumiza sana moyo wako iwe ni kazini, nyumbani au katika mahusiano.
Jambo la muhimu ni kujua namna ya kukabiliana na changamoto zote nzuri na mbaya, kwani ukiweka moyoni yale yanayo kuumiza huwezi kusonga mbele, ila ukiamua kusahau nakufanya juhudi katika maendeleo yako, basi utafanikiwa hata  wahenga walisema  " SAHAU YALIYOPITA UGANGE YAJAYO".
PANAPO MAJALIWA NDUGU ZANGUNI!

Sunday, January 15, 2017

JUMAPILI NJEMA KWA WOTE...AMANI NA FURAHA ZITAWALA KATIKA NYUMBA ZETU!

Zipo furaha nyingi duniani, watu wanafurahia kufaulu mitihani, kupata ajira, mtoto, kuoa na kuolewa, kuwa na mali nyingi na mambo mengi kadha wa kadha. Lakini hebu tuone furaha iliyo kuu kuliko zote, "Ndipo wale sabini  waliporudi kwa furaha wakisema hata pepo wanatutii, YESU akawambia msifurahi kwa vile pepo wanawatii BALI FURAHINI KWA SABABU MAJINA YENU YAMEANDIKWA MBINGUNI. Kumbe furaha kuu ni jina lako kuwa limeandikwa katika kitabu cha uzima. Luka 10:17-20".  JUMAPILI NJEMA.

Friday, January 13, 2017

TANZANIA TUNA NGOMA NYINGI SANA ZA ASILI...UNAKUMBUKA NGOMA HII YA MHAMBO?

Nakumbuka wakati nikiwa nikisoma shule ya msingi tulikuwa tukicheza ngoma zote za asili MUHAMBO ílikuwa mojawapo. na mwalimu wa ngoma hii namkumbka sana, aliitwa mwalimu Ndumbalo "Moyoumo" ...yaaani nimekumbuka sana ....pia nimetamani kwa hiyo nimecheza cheza hapa....PANAPO MAJALIWA NA NITAKULETEENI NGOMA NYINGINE YA ASILI:-) MWISHO WA JUMA UWE MWEMA NA MWENYE FURAHA NA AMANI...Kapulya

Thursday, January 12, 2017

HADITHI:- DALILI YA MVUA NI MAWINGU

Hii ni hadithi kuhusu kijana mmoja, aliyechagua msichana wa kumwoa, na kuzaa naye watoto, na kwa kali hiyo kuukuza ukoo wake. Lakini kabla ya mipango ya mwisho ya harusi na baba mkwe wake, aliamua awajaribu wakwe zake kwa mtihani mdogo.

Asubuhi moja, akaomba ruhusu kwa wake zake aende kijijini kwao akachukue vifaa vyake vya kulimia, na angeshukuru kama shemeji yake, dada wa atayekuwa mkewe atafuatana naye. "Umekuja hapa, kumtafuta mke utakayeishi naye, karibu tutakuwa ndugu, kwa hiyo shemeji yako akikubali, sisi hatuna kuzuizi," wakwe walimjibu.

Hivyo Kijana na shemeji yake wakaondoka, na walipofika kijijini kwake, badala ya kuchukua vifaa vya kilimo, akachukua mkuki, pamoja na shemeji yake, wakaenda kuwinda. Kijana akauwa mnyama mkubwa, wakaanza safari ya kurudi kijijini kwa wakwe zake. Shemeji yake akawa amebeba kitoweo huku kijana amebeba mkiku wake.

Njiani akamwambia shemeji yake, kuwa kuleta kitoweo nyumbani, ni njia mojawapo ya kuhakikisha uhodari na uwezo wa kuwatunza wakwe na familia yake. Wakapokewa kwa shangwe, kijana naye akapongezwa kwa uhodari wake.

Usiku huo huo, akawaeleza wakwe zake kwamba alitaka ajaribu tena jwenda kuwinda na vile vile akaomba ruhusu ya kufuatana na shemeji yake.
"Sasa tuko kama ndugu, sisi tunataka tukusaidie kwa kila njia tutavyoweza!" Baba mkwe akamwambia.

Hivyo, siku iliyofuata, wakaondoka tena na haikuchukua muda, kijana kwa uhodari wake, akauwa mnyama wapili. Mara hii mnyama aliyemwua alikuwa mkubwa na mzito kiasi kwamba, wote wawili walishindwa kumbeba. Uamuzi ukawa kwamba yule kijana, arudi kijijini kwenda kuomba msaada, na shemeji yake abakie kuchunga kitoweo. Kijana alipoondoka, yule msichana akapanda juu ya mti, kuhofia wanyama wakali, akisubiri msaada ufike.

Kijana alipofika kijijini akajitupa kwa kilio chini ya miguu ya mkewe wa mtarajiwa. Akisema kama amefanya kosa kubwa sana.
Badala ya kutupa mkuki kumchoma myama, sababu ya giza alimchoma dada yake ambaye sasa amemwacha amekufa porini.
Familia nzima wakajiwa na chuki na wakaanza kumtukana maneno mbali mbali, kusikia kisa hicho. Wakaanza kumpiga vile vile: " unawezaje kusema wewe ni mwindaji hodari, kutaka kutunza familia ikiwa umefanya upumbavu kama huu?" Walimpiga sana mpaka kidogo azirai. wakagundua kwamba wakiendelea kumpiga wanaweza kumuua na wasiweze kupata maiti ya msichana wao. Maana ni yule kijana peke yake alifahamu maiti ilipo. Wakamwamuru yule kijana ambaye alikuwa hai kwa mapigo, aongozane nao akawaonyeshe maiti ya msichana wao ilipo.

Walipofika, walistaajabu sana kumwona msichana wao akiteremka toka juu ya mti. Akishangaa na kuwauliza kwa nini yule kijana alikuwa katika hali mbaya hiyo huku ametapakaa damu. Familia nzima  ilishindwa kusema cho chote kuhusu kitendo hicho kwa kuona aibu, Kwa maovu waliyomfanyia. Wakamwomba msamaha yule kijana. Wakasaidiana kumchukua yule mnyama na kumkata vipande. Wakavibeba hivyo vipande na kurudi kijijini. Walipofika tu, yule kijana akafungasha mizigo yake na kabla hajaondoka, akawaambia kuwa hataoa msichana kutoka kwenye familia ya watu wasiokuwa na huruma na wakorofi.  Hivyo akafunga safari na kuondoka.

Haukupita muda, kwenye kijiji kingine alichohamia, akapata mchumba mwingine. Vile vile akawajaribu wakwe zake kama alivyofanya awali na mchumba wake wa kwanza. Safari hii mambo yakawa tofauti! Wakwe zake wapya, walishtuka na madhara yaliyotokea, akasamehewa kwa ajali iliyotokea na wakamwomba yule kijana akawaonyeshe sehemuu ambapo ajali ilitokea, ili wachukue maiti na kuja  kuzika ipasavyo. Walipofika sehemu ya ajali ilipotokea wakamkuta shemeji yake, yaani msichana wao mzima kabisa amesimama kando ya mnyama aliyeuawa na mkwe wao.

Ikabidi yule kijana aeleze mkasa toka mwanzo mpaka mwisho, akatoa sababu za kufanya kitendo hicho. Na kamaliza kusema kwamba, sasa amepata mke aliyekuwa  akimtafuta ambaye tabia yake pamoja na familia yake, ni ya watu adili. Akamuoa mchumba wake, wakaishi kwa muda kabla ya kuhamia kijijini kwa yule kijana na kuishi maisha yao yote
CHANZO:-  HADITHI NA VISA KUTOKA TANZANIA

Wednesday, January 11, 2017

UJUMBE MZURI KUTOKA KWA MAMA TERESA...

Kama unataka kubadilisha dunia hii nenda nyumbani na uipende famIlia yako. UJUMBE: Mama Teresa

Tuesday, January 10, 2017